Jumanne, 7 Julai 2015

DHANA NA SIFA ZA LUGHA

  • Lugha ni mfumo wa sauti nasibu zenye kubeba dhana na zilizokubaliwa na jamii ya watu katika eneo fulani ili ziendeleze mawasiliano baina yao.
                                                       Sifa za Lugha 
1. Sauti:
Lugha huambatana na sauti za binaadamu kutoka kinywani mwake. Binaadamu lazima atamke jambo kwa kutoa sauti, zinazotamkwa kwa utaratibu maalumu kutoka kwenye maumbile yaliyo ndani ya mwili wa mwanaadamu hususan kinywa, ambayo kiisimu huitwa ala za sauti.
2. Lugha ni lazima imhusu MwanadamuKimsingi hakuna kiumbe kisichokuwa mwanaadamu (mtu) kinachoweza kuzungumza Lugha. Lugha ni chombo maalumu wanachokitumia binaadamu kwa lengo la mawasiliano. 
3. Lugha huzingatia utaratibu maalum;Sauti za lugha yoyote huwa zimepangwa kwa kufuata utaratibu fulani  unaokubaliwa
na jamii ya watu wanaotumia lugha inayohusika.  Kwa maneno mengine, si kila sauti
itokayo kinywani mwa mwanaadamu kuwa ni lugha. Sauti za vilio vya watoto, hoi
hoi na vigeregere vya waliofurahi, vikohozi vya wagonjwa wa pumu na vifua,
vicheko, sauti za kupenga kamasi, pinja na kelele nyenginezo haziwezi kuitwa lugha.
Utaratibu huo maalumu unaofuatwa na lugha za wanaadamu huitwa sarufi.
4.Lugha hufuata misingi ya fonimu Wanaisimu wanakubaliana kwa ujumla kwamba fonimu ni sauti yenye uwezo wa
kuleta tofauti katika maana ikipachikwa katika neno la lugha husika. Dhana ya
fonimu inatarajiwa kuzungumziwa kwa kirefu sana katika muhadhara wa sabaa. Kwa
mfano baadhi ya fonimu za Kiswahili ni .
/a/, /e/, /i/, /o/, /u/, kama zinavyoweza kubadilisha maana katika maneno
yafuatayo:-/tata/~ /teta/~/tita/~/tota/~ /tuta/.
/p/, /b/, /t/, /d/, /c/, /k/, /g/, /s/, /z/. kama zinavyoweza kubadilisha maana
katika maneno yafuatayo:-pawa~ bawa~ tawa~ dawa~ chawa~ jawa~ kawa~ sawa~ zawa, n.k
  Lugha hufuata mpangilio wa vipashio unaoleta maana
Muundo wa Lugha huwa unafuata mpangilio wa vipashio vyake maalumu na
lazima vipashio hivyo vifahamike. Mpangilio wa vipashio huo huanza na
fonimu, neno ambalo huundwa kwa mkusanyiko wa silabi au muunganiko wa
mofimu mbalimbali, kirai, kishazi na sentensi
.5 Lugha inajizalishaVipashio vinavyoiunda lugha husika huwa na sifa ya kuweza kunyumbulishwa ili
kupata maneno mapya. Kwa mfano vitenzi hunyambulishwa kwa kuongezwa
viambishi nz kwa hivyo, lugha hujiongezea maneno mapya. Kwa mfano tuangalie
mifano ifuatayo.
i)   chez-a-------ku-chez-a-------ku-m-chez-a-------tu-li-m-chez-a.
ii)   chez-e-a-------chez-ek-a----------chez-e-an-a-------chez-esh-a-------chez-w-a
iii)   chez-esh-a- chez-esh-an-a- chez-esh-e-an-a
  Lugha husharabu
Lugha husharabu kwa maana ya  kwamba huchukuwa maneno kutoka lugha
nyengine ili kujiongezea msamiati wake.Tabia hii inazisaidia sana Lugha
zinazokua. 
                            Tabia za Lugha
  Lugha ina tabia ya kukua
Lugha hukua kadiri inavyoendelea kutumiwa na jamii. Kukua kwa Lugha
kuna vigezo kadhaa vinavyozingatiwa. Miongoni mwa vigezo hivyo ni
kubadilika na kuongezeka kwa msamiati wa Lugha hiyo. Maneno ya zamani
yanabadilika na maneno mapya yanaingia katika Lugha mbalimbali. Hii ni
kutokana na mahitaji ya umma au jamii katika harakati mbali mbali
yanayotokana na maendeleo ya ulimwengu kwenye njanja tofauti tofauti
zikewemo za kiuchumi, kisiasa, kisayansi na kiteknolojia.Tukichukua mfano
wa Lugha ya Kiswahili, tunagundua maneno mengi ambayo yameingia
kwenye Lugha hii kwa sababu kadhaa. Baadhi ya maneno ambayo sasa hivi
yanatumika katika Kiswahili ambayo miaka kama kumi nyuma hayakuwemo
katika Lugha ya Kiswahili ni pamoja na kasheshe, dingi, miundombinu,
mikakati,mdau, ngangari na mengi mengineyo. Kuongezeka kwa watumiaji
pia ni kigezo chengine kinachoashiria kukua kwa Lugha ambacho kinaenda
sambamba na kigezo cha kutanuka na kuongezeka maeneo ambapo lugha hiyo
inatumiwa.
  Lugha ina tabia ya kuathiri na kukubali kuathiriwa.
Lugha inaweza kuathiri na kuathiriwa na Lugha nyengine .Mfano lugha ya
Kiswahili imeathiriwa sana na Lugha za Kiarabu, Kiingereza na hata Lugha za
Kibantu. Yawezekana pia kwa kiasi fulani ikawa Kiswahili kimeziathiri
Lugha hizo. Mfano wa maneno yenye asili ya Kiarabu ambayo yameingia
katika Lugha ya Kiswahili ni kalamu, kitabu, daftari, adhadu, thawabu,
dhambi, dhahabu, sababu,aibu, laana, zina, dhima, wajibu, mahaba,sakafu,
karibu, tafadhali,nafsi, roho, safari, salamu, amali, tabia, sifa, n.k. Mfano wa
maneno yenye asili ya Kiingereza yaliyoingia katika Kiswahili ni buku, peni,
begi, kabati, rula, buti,bia,springi, stoo, skrubu ,n.k .Mfano wa maneno yenye
asili ya Lugha za Kibantu ni pamoja na  ikulu  kutoka lugha za Kigogo,
Kisukuma na Kinnyamwezi, bunge kutoka katika lugha za Kigogo, Kisambaa,
Kiha na Kiganda, ugiligili  kutoka katika lugha ya Kinyakyusa,  ngowela
kutoka katika lugha ya Kikaguru, Kitivo kutoka katika lugha Kipare na
Kisambaa,  kivunge  kutoka katika lugha ya Kipare,  unga  kutoka katika lugha
ya kizigua na misamiati mingi mingineyo kutoka lugha tofauti tofauti za
kibantu.
  Ubora wa lugha 
Lugha zote ni bora. Hakuna lugha iliyo bora zaidi kuliko lugha nyengine. Ubora
wa lugha upo kwa wale wanaoitumia.
  Kujitosheleza
Kila lugha inajitosheleza kulingana na mahitaji ya jamii ambayo inatumia
lugha yenyewe katika kipindi husika cha maisha yake 
                                Dhima za Lugha
  Ujumi:
ujumi ni hali ya kutumia maneno ya lugha fulani kwa ufundi na ustadi
wa hali ya juu kwa lengo la kuburudisha na kuwavutia watu wengine. Baadhi
ya watu hutumia lugha kwa dhima hiyo, ili maksudi wasomaji au wasikilizaji
wao wavutike na kuburudishwa na Lugha hiyo. Maeneo yatumikamo lugha
yenye  ujumi  wa kiwango cha juu ni kwenye matangazo na kwenye fani ya
utunzi wa mashairi.
  Utambuzi: 
Ni hali ya kufikiria kwa makini, kukokotoa na kutoa majibu ya
maswali tofauti ndani ya ubongo. Chombo kikuu kitumikacho kutoa majibu
hayo ni lugha. Kutokana na muktadha huo tunaweza kusema kwamba lugha
hutumika kama chombo cha utambuzi.
  Hisia: 
ni fikra  za ndani alizokuwa nazo kiumbe mwanaadamu. Tunapotaka
kuonyesha  hisia  zetu na vilevile kuwavuta wengine kwa maneno mazito
yanayoweza kumtoa msikilizaji machozi ya huzuni au ya furaha tunachagua
maneno makali yenye hisia.
  Kujielezea: 
Hali ya mtu kudhihirisha mambo mbalimbali aliyokuwa nayo
ndani ya moyo wake. Kwa mfano mtu anaposema nina furaha sana. Hapa mtu
anatowa msisitizo wa kuonyesha kiwango cha furaha alichonacho, hili
linafanyika kwa kutumia lugha. kwa ufupi tunachoweza kusema hapa ni
kwamba lugha hutumika kwa ajili ya kujielezea.
  Kuamuru: 
Ni kutoa maelekezo kwa njia ya kuamrisha. Kwa mfano jaji
anamuhukumu mshitakiwa kwa  kumuamuru ‘Ninakufunga miaka mitatu
jela’. Hapa lugha inatenda kazi ya kuamuru.
  Kushirikiana:
ni hali ya kutenda kitu kwa pamoja  au hali ya kuwa na ubiya
kwenye jambo. Lugha huwezesha watu kujenga mahusiano ya siri baina ya
watu wawili au zaidi na kuweza kujitengenezea njia zao za kuwasiliana pasina
wengine kuelewa.
  Kuonesha: 
kumuelekeza mtu kitu kwa njia ya kuashiria. Unapotaka
kuonesha jambo ni lazima utumiye lugha kwa nija moja au nyengine. 
                            Matumizi na umuhimu wa Lugha
  Kuwasiliana:- 
Lugha hutumika kupashana habari
  Kuunganisha-  Lugha hupatanisha na kuleta uelewano miongoni mwa wana
jamii. pia lugha huweza kutofautisha  jamii moja na nyengine.
  Kujenga jamii- lugha huleta/huhimiza shughuli za maendeleo ya jamii, huleta
amani na mshikamano katika jamii.
  Kufundishia- Lugha hutumika katika kufundishia elimu.
  Kutambulisha- Lugha hutumika kutambulisha jamii ya watu Fulani.
  Kuhifadhi- Lugha ndicho chombo cha kuhifadhi na kueneza utamadun.

Maoni 14 :

  1. Tunashukuru sana kwa muhtasari wa mada hizi

    JibuFuta
  2. Nashukuru kwa maelezo kuhusu dhana ya lugha nimejifunza mengi. Assnte

    JibuFuta
  3. kazi kuntu endelea vivyo hivyo

    JibuFuta
  4. Nawashukuru wanazuoni wa lugha yetu adhimu ya Kiswahili maana mmenipa uelewa baada ya kudurusu

    JibuFuta
  5. Asante kwa ujuzi huu nisiwokuwa naujua hapo awali

    JibuFuta
  6. Ahsante umenisaidia nilikua sijui ila sasa nimejua kwanza nimegoogle nikiwa class 😂😂😂😂😂😂

    JibuFuta