Jumanne, 7 Julai 2015

DHANA NA SIFA ZA LUGHA

  • Lugha ni mfumo wa sauti nasibu zenye kubeba dhana na zilizokubaliwa na jamii ya watu katika eneo fulani ili ziendeleze mawasiliano baina yao.
                                                       Sifa za Lugha 
1. Sauti:
Lugha huambatana na sauti za binaadamu kutoka kinywani mwake. Binaadamu lazima atamke jambo kwa kutoa sauti, zinazotamkwa kwa utaratibu maalumu kutoka kwenye maumbile yaliyo ndani ya mwili wa mwanaadamu hususan kinywa, ambayo kiisimu huitwa ala za sauti.
2. Lugha ni lazima imhusu MwanadamuKimsingi hakuna kiumbe kisichokuwa mwanaadamu (mtu) kinachoweza kuzungumza Lugha. Lugha ni chombo maalumu wanachokitumia binaadamu kwa lengo la mawasiliano. 
3. Lugha huzingatia utaratibu maalum;Sauti za lugha yoyote huwa zimepangwa kwa kufuata utaratibu fulani  unaokubaliwa
na jamii ya watu wanaotumia lugha inayohusika.  Kwa maneno mengine, si kila sauti
itokayo kinywani mwa mwanaadamu kuwa ni lugha. Sauti za vilio vya watoto, hoi
hoi na vigeregere vya waliofurahi, vikohozi vya wagonjwa wa pumu na vifua,
vicheko, sauti za kupenga kamasi, pinja na kelele nyenginezo haziwezi kuitwa lugha.
Utaratibu huo maalumu unaofuatwa na lugha za wanaadamu huitwa sarufi.
4.Lugha hufuata misingi ya fonimu Wanaisimu wanakubaliana kwa ujumla kwamba fonimu ni sauti yenye uwezo wa
kuleta tofauti katika maana ikipachikwa katika neno la lugha husika. Dhana ya
fonimu inatarajiwa kuzungumziwa kwa kirefu sana katika muhadhara wa sabaa. Kwa
mfano baadhi ya fonimu za Kiswahili ni .
/a/, /e/, /i/, /o/, /u/, kama zinavyoweza kubadilisha maana katika maneno
yafuatayo:-/tata/~ /teta/~/tita/~/tota/~ /tuta/.
/p/, /b/, /t/, /d/, /c/, /k/, /g/, /s/, /z/. kama zinavyoweza kubadilisha maana
katika maneno yafuatayo:-pawa~ bawa~ tawa~ dawa~ chawa~ jawa~ kawa~ sawa~ zawa, n.k
  Lugha hufuata mpangilio wa vipashio unaoleta maana
Muundo wa Lugha huwa unafuata mpangilio wa vipashio vyake maalumu na
lazima vipashio hivyo vifahamike. Mpangilio wa vipashio huo huanza na
fonimu, neno ambalo huundwa kwa mkusanyiko wa silabi au muunganiko wa
mofimu mbalimbali, kirai, kishazi na sentensi
.5 Lugha inajizalishaVipashio vinavyoiunda lugha husika huwa na sifa ya kuweza kunyumbulishwa ili
kupata maneno mapya. Kwa mfano vitenzi hunyambulishwa kwa kuongezwa
viambishi nz kwa hivyo, lugha hujiongezea maneno mapya. Kwa mfano tuangalie
mifano ifuatayo.
i)   chez-a-------ku-chez-a-------ku-m-chez-a-------tu-li-m-chez-a.
ii)   chez-e-a-------chez-ek-a----------chez-e-an-a-------chez-esh-a-------chez-w-a
iii)   chez-esh-a- chez-esh-an-a- chez-esh-e-an-a
  Lugha husharabu
Lugha husharabu kwa maana ya  kwamba huchukuwa maneno kutoka lugha
nyengine ili kujiongezea msamiati wake.Tabia hii inazisaidia sana Lugha
zinazokua. 
                            Tabia za Lugha
  Lugha ina tabia ya kukua
Lugha hukua kadiri inavyoendelea kutumiwa na jamii. Kukua kwa Lugha
kuna vigezo kadhaa vinavyozingatiwa. Miongoni mwa vigezo hivyo ni
kubadilika na kuongezeka kwa msamiati wa Lugha hiyo. Maneno ya zamani
yanabadilika na maneno mapya yanaingia katika Lugha mbalimbali. Hii ni
kutokana na mahitaji ya umma au jamii katika harakati mbali mbali
yanayotokana na maendeleo ya ulimwengu kwenye njanja tofauti tofauti
zikewemo za kiuchumi, kisiasa, kisayansi na kiteknolojia.Tukichukua mfano
wa Lugha ya Kiswahili, tunagundua maneno mengi ambayo yameingia
kwenye Lugha hii kwa sababu kadhaa. Baadhi ya maneno ambayo sasa hivi
yanatumika katika Kiswahili ambayo miaka kama kumi nyuma hayakuwemo
katika Lugha ya Kiswahili ni pamoja na kasheshe, dingi, miundombinu,
mikakati,mdau, ngangari na mengi mengineyo. Kuongezeka kwa watumiaji
pia ni kigezo chengine kinachoashiria kukua kwa Lugha ambacho kinaenda
sambamba na kigezo cha kutanuka na kuongezeka maeneo ambapo lugha hiyo
inatumiwa.
  Lugha ina tabia ya kuathiri na kukubali kuathiriwa.
Lugha inaweza kuathiri na kuathiriwa na Lugha nyengine .Mfano lugha ya
Kiswahili imeathiriwa sana na Lugha za Kiarabu, Kiingereza na hata Lugha za
Kibantu. Yawezekana pia kwa kiasi fulani ikawa Kiswahili kimeziathiri
Lugha hizo. Mfano wa maneno yenye asili ya Kiarabu ambayo yameingia
katika Lugha ya Kiswahili ni kalamu, kitabu, daftari, adhadu, thawabu,
dhambi, dhahabu, sababu,aibu, laana, zina, dhima, wajibu, mahaba,sakafu,
karibu, tafadhali,nafsi, roho, safari, salamu, amali, tabia, sifa, n.k. Mfano wa
maneno yenye asili ya Kiingereza yaliyoingia katika Kiswahili ni buku, peni,
begi, kabati, rula, buti,bia,springi, stoo, skrubu ,n.k .Mfano wa maneno yenye
asili ya Lugha za Kibantu ni pamoja na  ikulu  kutoka lugha za Kigogo,
Kisukuma na Kinnyamwezi, bunge kutoka katika lugha za Kigogo, Kisambaa,
Kiha na Kiganda, ugiligili  kutoka katika lugha ya Kinyakyusa,  ngowela
kutoka katika lugha ya Kikaguru, Kitivo kutoka katika lugha Kipare na
Kisambaa,  kivunge  kutoka katika lugha ya Kipare,  unga  kutoka katika lugha
ya kizigua na misamiati mingi mingineyo kutoka lugha tofauti tofauti za
kibantu.
  Ubora wa lugha 
Lugha zote ni bora. Hakuna lugha iliyo bora zaidi kuliko lugha nyengine. Ubora
wa lugha upo kwa wale wanaoitumia.
  Kujitosheleza
Kila lugha inajitosheleza kulingana na mahitaji ya jamii ambayo inatumia
lugha yenyewe katika kipindi husika cha maisha yake 
                                Dhima za Lugha
  Ujumi:
ujumi ni hali ya kutumia maneno ya lugha fulani kwa ufundi na ustadi
wa hali ya juu kwa lengo la kuburudisha na kuwavutia watu wengine. Baadhi
ya watu hutumia lugha kwa dhima hiyo, ili maksudi wasomaji au wasikilizaji
wao wavutike na kuburudishwa na Lugha hiyo. Maeneo yatumikamo lugha
yenye  ujumi  wa kiwango cha juu ni kwenye matangazo na kwenye fani ya
utunzi wa mashairi.
  Utambuzi: 
Ni hali ya kufikiria kwa makini, kukokotoa na kutoa majibu ya
maswali tofauti ndani ya ubongo. Chombo kikuu kitumikacho kutoa majibu
hayo ni lugha. Kutokana na muktadha huo tunaweza kusema kwamba lugha
hutumika kama chombo cha utambuzi.
  Hisia: 
ni fikra  za ndani alizokuwa nazo kiumbe mwanaadamu. Tunapotaka
kuonyesha  hisia  zetu na vilevile kuwavuta wengine kwa maneno mazito
yanayoweza kumtoa msikilizaji machozi ya huzuni au ya furaha tunachagua
maneno makali yenye hisia.
  Kujielezea: 
Hali ya mtu kudhihirisha mambo mbalimbali aliyokuwa nayo
ndani ya moyo wake. Kwa mfano mtu anaposema nina furaha sana. Hapa mtu
anatowa msisitizo wa kuonyesha kiwango cha furaha alichonacho, hili
linafanyika kwa kutumia lugha. kwa ufupi tunachoweza kusema hapa ni
kwamba lugha hutumika kwa ajili ya kujielezea.
  Kuamuru: 
Ni kutoa maelekezo kwa njia ya kuamrisha. Kwa mfano jaji
anamuhukumu mshitakiwa kwa  kumuamuru ‘Ninakufunga miaka mitatu
jela’. Hapa lugha inatenda kazi ya kuamuru.
  Kushirikiana:
ni hali ya kutenda kitu kwa pamoja  au hali ya kuwa na ubiya
kwenye jambo. Lugha huwezesha watu kujenga mahusiano ya siri baina ya
watu wawili au zaidi na kuweza kujitengenezea njia zao za kuwasiliana pasina
wengine kuelewa.
  Kuonesha: 
kumuelekeza mtu kitu kwa njia ya kuashiria. Unapotaka
kuonesha jambo ni lazima utumiye lugha kwa nija moja au nyengine. 
                            Matumizi na umuhimu wa Lugha
  Kuwasiliana:- 
Lugha hutumika kupashana habari
  Kuunganisha-  Lugha hupatanisha na kuleta uelewano miongoni mwa wana
jamii. pia lugha huweza kutofautisha  jamii moja na nyengine.
  Kujenga jamii- lugha huleta/huhimiza shughuli za maendeleo ya jamii, huleta
amani na mshikamano katika jamii.
  Kufundishia- Lugha hutumika katika kufundishia elimu.
  Kutambulisha- Lugha hutumika kutambulisha jamii ya watu Fulani.
  Kuhifadhi- Lugha ndicho chombo cha kuhifadhi na kueneza utamadun.

MAKUNDI NENO KATIKA KISWAHILI

KIRAI

Ni kipashio cha lugha ambacho huwa na muundo wa neno moja au zaidi lakini huwa hakina muundo wa kiima na kiarifu. Muundo wa kirai huwa ni wa neno moja au zaidi ambayo huwa pamoja katika mpangilio maalumu wenye kuzingatia uhusiano wa maneno hayo na neno kuu ambalo ndio huwa linabeba aina ya kundi hilo la maneno.
            AINA ZA VIRAI
A.    Kirai nomino (KN)
Hili ni kundi la maneno ambalo hutawaliwa na nomino. Kirai nomino huundwa na maneno yafuatayo:-
o   Nomino pekee. Mfano; Asha anapika, Nyangoye anaimba, Nyegera anacheza (N)
o   Nomino mbili au zaidi zinazounganishwa. Mfano; Mhindi na Sagati wanacheza. (N+U+N)
o   Nomino na kivumishi. Mfano; Mtoto mnene amekuja, Mzee mfupi ameondoka. (N+V)
o   Kiwakilishi pekee. Mfano; Yule ameondoka, Wewe umenena, Wale waliokuja. (W)
o   Kiwakilishi na kivumishi. Mfano; Yule mvivu amerudi, Wewe mlemavu njoo. (W+V)
o   Nomino na kitenzi jina. Mfano; Mchezo wa kusisimua, Wimbo wa kupendeza. (N+Ktj)
o   Nomino na kishazi tegemezi kivumishi. Mfano; Mjukuu aliyepotea, Mheshimiwa aliyeondoka. (N+βV)
B.     Kirai kivumishi (KV)
Hiki ni kirai ambacho muundo wake umejikita katika kivumishi na maneno yanayohusiana na kivumishi katika tungo tungo hiyo. Virai hivi kwa kawaida hujibainisha zaidi kimuundo kama sehemu ya virai nomino. Virai hivi huundwa na:-
o   Kivumishi na Kirai nomino. Mfano; Mwenye mali nyingi, Wenye watoto wengi.
o   Kivumishi na kielezi. Mfano; Mzuri sana, Mweupe pee!,Mweusi tii!, Mbaya sana.
o   Kivumishi na kirai kitenzi. Mfano; Mwenye kupiga gitaa, Mwenye kupenda sana.
o   Kivumishi na kirai kiunganishi. Mfano; Nzuri ya kupendeza, Mpungufu wa akili.
C.    Kirai kitenzi (KT)
Ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi, au katika uhusiano wa kitenzi na neno au mafungu ya mengine ya maneno. Hii ina maana kwamba, neno kuu katika kirai hiki ni kitenzi. Kirai kitenzi kimeundwa na vipashio vifuatavyo:-

o   Kitenzi pekee. Mfano; amekuja, amekula, ameoga. (T)
o   Kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu. Mfano; Alikua anacheza(Ts+T), Alikua anaweza kuimba. (Ts+Ts+T)
o   Kitenzi kishirikishi na shamirisho. Mfano; Ni mtanashati, Ndiye mwizi, Sio mwelewa. (t+sh)
o   Kitenzi, jina na kielezi. Mfano; Nimepika uji asubuhi
D.    Kirai kielezi
Tofauti na aina nyingine ya virai, miundo ya virai vielezi haielekei kukitwa kwenye mahusiano ya lazima baina ya neno kuu (yaani kielezi ) na neno au fungu la maneno linaloandamana nalo. Badala yake miuundo inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika Lugha kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua zaidi neno hilo. Zaidi kirai kielezi huelezea namna, wakati, mahali na kinachofanya tendo hilo litendeke. Mfano; Mara nyingi, Sana sana, Polepole, Jana asubuhi, Kesho mchana, n.k.
E.     Kirai kihusishi
Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika mahusiano baina ya vihusishikwa, na, katika,au kwenye na fungu la maneno linaloandamana nacho. Kwa maneno menginekirai hicho ni kile ambacho neno kuu ni kihusishi. Virai vihusishi japokuwa muundo wake hufanana ila hutofautiana kimaana, zipo maana tatuambazo ni:-
a)      Pahala – kwa baba, katika kabati, kwenye lindo
b)      Utumizi – Kwa kisu, Kwa mkono
c)      Uhusika – Na Mjomba, Na Bibi.
Vilvile kirai kihusishi hutumiwa kutekeleza majukumu yafuatayo katika sentensi:-
ü  Kama kivumishi. Mfano; Penseli ya mjomba, Mkoba wa mama, Koti la babu
ü  Kama kielezi. Mfano; Tulisikiliza kwa makini, Tuliimba kwa shangwe, Tulisoma kwa juhudi
ü  Kama kiwakilishi. Mfano; La mjomba limetupwa, Ya shangazi imeuzwa, Wa nne ameondoka

TABIA ZA VITENZI VYA KISWAHILI

  • Vitenzi vya Kiswahili huwa na tabia tofauti tofauti zinazotokana na dhima za mofimu ambazo hupachikwa katika vitenzi hivyo, hivyo kulingana na dhima za mofimu, vitenzi vya Kiswahili huwa na tabia zifuatazo:-
   I.               Kutambulisha nafsi. Mfano:- Anayesoma
    II.            Kutambulisha tendo. Mfano:- Cheza, Lima, Imba n.k.
III.            Kutambulisha wakati. Mfano:- Ulikuja 
 IV.            Kutambulisha hali ya uyakinishi na ukanushi. Mfano:- Anacheka – Hacheki 
   V.            Kutambulisha kauli mbalimbali za tendo. Mfano:- cheza-chezwa-chezewa-chezeka n.k.
VI.            Kutambulisha hali za nakati katika tendo. Mfano:-Huimba, Amekula. 
VII.            Kuonesha urejeshi wa mtenda, mtendwa na mtendewa ambao hujidhihirisha katika ngeli ya nomino iliyotajwa kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi. Urejeshi huo ni wa O-rejeshi. Katika urejeshi huo vitenzi hubeba viambishi ngeli vya –O- isipokuwa kama nomino ni ya ngeli ya kwanza umoja  ambapo hutumia –e- badala ya –O-.
Mfano:-
NGELI
KIAMBISHI CHA O- REJESHI
MFANO
A-WA
-YE- na –O-
Aliyepiga / Waliokuja
U-I
-O- na –YO-
Uliokatwa / Iliyokatwa
LI-YA
-LO- na –YO-
Lililochanika / Yaliyochanika
KI-VI
-CHO- na –VYO-
Kilichovunjika / Vilivyovunjika
I-ZI
-YO- na –ZO-
Iliyofungwa / Zilizofungwa
U-ZI
-O- na -ZO
Uliokatika / Zilizokatika
U-YA
-O- na –ZO-
Ulionipata / Yaliyonipata
KU
-KO-
Kulikotokea
PA-MU-KU
PO-MO-KO
Pale alipoingia / Mule alimotokea / Kule alikofunga

MOFIMU



Mofimu ni kipashio kidogo kabisa cha lugha ambacho kina uwezo wa kusitiri maana ya neno ambalo kwalo limeundwa. AU ni kipashio kidogo kabisa cha lugha chenye maana kisarufi.

                                    AINA ZA MOFIMU
Mofimu huru ni aina ya mofimu ambayo huweza kusimama pekee na kujitosheleza kimaana yaani huwa na sifa ya neno. Mfano; mama, Baba, Dada, Kaka, Mjomba, Shangazi n.k. Kwa mifano hiyo utagundua kuwa mofimu huru haziwezi kugawanyika zaidi na kubeba maana kisarufi, kwa maana kwamba mofimu ‘baba’ ikigawanywa ba-ba, ‘ba’ hii haina maana yoyote kisarufi zaidi ya kuwa silabi.

Mofimu tegemezi ni aina ya mofimu ambayo huweza kuvunjwavunjwa na kubeba maana kisarufi, mofimu tegemezi hutegemeana ili kuleta maana kamili ya neno.
Mfano; neno ‘anakula’ limeundwa na mofimu zifuatazo:- [a-na-kul-a] ambazo kila moja hubeba dhana Fulani ya kisarufi.

VIAMBISHI
            Ni mofimu zinazopachikwa nyuma au mbele ya mzizi wa neno ili kubadilisha dhana ya neno. Kwa kuwa mofimu hizo hupachikwa sehemu tatu tofauti, tunapata aina tatu za viambishi kwa mujibu wa nafasi zake katika neno, yaani; viambishi awali ambavyo hupachikwa mwanzoni au nyuma ya mzizi wa neno,viambishi kati ambavyo hupachikwa katikati ya neno (Kiswahili hakina viambishi hivi) na viambishi tamati ambavyo hivi hupachikwa mbele au mwishoni mwa mzizi wa neno.
Mfano:-
VIAMBISHI AWALI
MZIZI WA NENO
VIAMBISHI TAMATI
NENO JIPYA
    A
    na
           chez
     ew
    a
Anachezewa
    Wa
     li
           chez
     ean
    a
Walichezeana
    Tu
    ta
           chez
     e
    a
Tutachezea


1.      Viambishi awali Hivi hupachikwa kabla ya mzizi wa neno na huwa ni vya aina tisa:-
i.                    Viambisha awali vya nafsi- hivi hudokeza upatanishi wa  nafsi katika kitenzi, zipo nafsi tatu, nafsi ya kwanza, ya pili, naya tatu.

NAFSI
UMOJA
UWINGI
Ya Kwanza
Ni-
Tu-
Ya Pili
U-
M-
Ya Tatu
A-
Wa-



M


Mfano:-Ninalima
            Tunacheza

ii.                  Viambishi awali vya ngeli- hivi hupatikana mwanzoni mwa nomino au vivumishi ili kudokeza hali ya umoja na uwingi.

Mfano:-Mtu (umoja) – Watu (uwingi)
            Msafi (umoja) – Wasafi (uwingi)

iii.                Viambishi awali vya ukanushi - hivi hudokeza hali ya uhasi wa tendo. Huwakilishwa na mofimu (ha-) na (si-)

Mfano:- Amekula (uyakinifu) – Hajala (ukanushi), Nakula (uyakinifu) – Sili (ukanushi)
iv.                Viambishi awali vya Njeo- hivi hudokeza nyakati mbalimbali ambazo ni wakati uliopita, uliopo na ujao.

NYAKATI
MOFIMU
Uliopo
-Na-
Uliopita
-li-
Ujao
-Ta-

            Mfano:- Mlituona
                          Utakuja

v.                  Viambishi awali vya hali- hivi hudokeza hali mbili za nyakati ambazo ni mazoea ambayo huwakilishwa na mofimu {hu} na timilifu inayowakilishwa na mofimu {me}.
Mfano:-Hucheza
              Amelima

vi.                Viambishi awali vya masharti-hivi hudokeza hali ya masharti au uwezekano katika tendo. Mofimu hizo ni kama –ki-, nge-, ngali- n.k.

Mfano:- ukija
              Ungekuja
               Angalimkuta

vii.              Kiambishi cha urejeshi wa mtenda (kiima)- mhiki hudokeza urejeshi wa nomino inayotenda katika kitenzi.

Mfano: - Aliyekuja {-ye-} hudokeza urejeshi wa mtenda.

viii.            Kiambishi kiwakilishi cha mtendwa au mtendewa (shamirisho) – hivi huwakilisha mtendwa au mtendewa wa jambo.
Mfano; Nilimpiga, Uliukata, Nimeipenda, Wameniteta.

ix.                Kiambishi awali cha kujirejea (kujitendea) – hiki huwakilishwa na mofimu (-ji-)
Mfano; kujipenda

2.      Viambishi tamati– Hivi hudokeza kauli mbalimbali za vitenzi.
Mfano: - Anacheza – kutenda
Unachezwa- Kutendwa
              Utachezewa- Kutendewa
               Nimemlia- Kutendea
              Wamewasomesha- Kutendesha n.k

Mzizi
Kiambishi cha Kauli
Kiambishi tamati maana
Neno jipya
Kauli
Viambishi vya kauli
Chez

a
Cheza
Kutenda
-a

e
a
Chezea
kutendea
-e-
Pig
ian
a
Pigiana
Kutendeana
-ian-/-ean-

iw
a
Pigiwa
Kutendewa
-iw-/ew-
Som
esh
a
Somesha
Kutendesha
-ish-/esh-

eshw
a
Someshwa
Kutendeshwa
-ishw-/eshw-
Lim
ik
a
Limika
Kutendeka
-ik-/-ek-

an
a
Limana
Kutendana
-an-

w
a
Limwa
Kutendwa
-w-

DHANA YA MZIZI NA SHINA LA KITENZI

Mzizi wakitenzini sehemu ya neno inayobakia mara baada ya kuondoa viambishi vyote vya awali na tamati katika neno hilo. Mfano: - a-na-chez-a {-chez-}, m-ku-lim-a {-lim-}
Mzizi fungeni ule ambao hauwezi kujikamilisha kimaana yaani hauwezi kusimama kama neno. Mfano; -lim-, -chez-, -imb- n.k.
Mzizi huruni ule ambao huweza kusimama kama neno na ukichanganuliwa zaidi hupoteza maana yake ya msingi. Mfano; Kinu, Kazi, Arifu, Sali n.k.


Shina la kitenzi ni sehemu ya neno ambayo huongezwa viambishi fuatishi (tamati) au ni sehemu ya neno ambayo hubakia baada ya kuondolewa viambishi tangulizi. Mfano:- chez+a = cheza, lim+a = lima. Sehemu hii ya neno hutumika kuundia neno jipya.
Shina sahili – hili ni shina ambalo huundwa na mofimu moja tu ambayo ni mzizi wa neno hilo, huwa ni mofimu huru, Mfano; Kesho, jana, kitabu, jarida n.k.
Shina changamano – shina hili huundwa na mzizi na kiambishi tamati maana. Mfano; cheka, lala, lia, kula n.k
Shina ambatani – shina hili huundwa na mofimu mbili ambazo ni huru. Mfano; mwana + kwenda = mwanakwenda, mbwa + mwitu = mbwamwitu