Alhamisi, 5 Mei 2016

CHIMBUKO NA ASILI YA KISWAHILI

ASILI YA KISWAHILI Yako maneno mawili ambayo tunayochanganya katika matumizi nayo ni asili ya lugha ya Kiswahili na chimbuko lake. Neno asili lina maana ya jinsi jambo lilivyoanza au lilivyotokea. Ama kwa neno chimbuko, maana yake ni mahalikitu au jambo lilipoanza. Kwa hiyo asili na chimbuko yanatofautiana katika maana.Zimewahi kutokea nadharia kadhaa kuhusu asili ya Kiswahili ambazo nitazieleza hivi punde. Kwanza ipo nadharia kuwa Kiswahili kimetokana na lugha ya Kiarabu. Pili iko nadharia kuwa Kiswahili ni mchanganyiko wa Kiarabu na lugha za Kibantu zilizotumika katika upwa wa Afrika Mashariki. Tatu, ni kuwa Kiswahili nilugha ya Kibantu iliyoathiriwa sana na Kiarabu hasa kimsamiati. Nne, Kiswahili kilitokana na mchanganyiko wa lugha kadhaa za Kibantu zilizokuwa katika upwa wa Afrika Mashariki.Nadharia isemayo kuwa Kiswahili kilitokana na Kiarabu inaegemea sana wingi wa maneno yenye asili ya Kiarabuna pia dini ya Kiislamu. Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianza pwani na kwa kuwa idadi kubwa ya wananchi wa pwani ni Waislamu na kwa kuwa Uislamu uliletwa na Waarabu, basi Kiswahili nacho kinashabihiana na Kiarabu. Madai haya hayana mashiko kwani Kiswahili ni lughakamili iliyokopa maneno kutoka katika lugha za Kiarabu, Kiajemi, Kireno, Kihindi, Kijerumani na Kiingereza kutokana na mawasiliano ya karne nyingi kati ya wenyeji wa pwani na wafanyabiashara wa kigeniUchunguzi uliofanywa na wataalamu waKiswahili hasa wanaisimu wamegundua kuwa mabadiliko yalihusu msamiati tu na wala siyo maumbo ya maneno wala miundo ya tungo za Kiswahili. Ikumbukwe pia kwamba uchunguzi ulikwishafanywa kuwa kwa kipindi kirefuKiswahili kilitumia maneno mengi kutoka katika lugha za Kibantu kwa kuwa wasemaji wengi wa Kiswahili ni Wabantu.Jambo la msingi ni kuwa lugha kuwa na maneno mengi ya kukopa kutoka katika lugha nyingine haifanyi lugha hiyo ionekaneimetokana na hiyo lugha ngeni. Inabidi kuzingatia zaidi msingi wa lugha kwa upande wa fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia ya lugha husika. Kimsingi, vigezo pekee vinavyoweza kutumika ili kuibainisha lugha ni vya kisimu kama vilefonolojia, mofolojia na sintaksia lakini msamiati siyo msingi pekee wa kuzingatia.Nadharia ambazo zinazaweza kuwa ni msingi wa uhakika ni mbili. Moja ni ile isemayo kuwa Kiswahili kina asili ya Kibantu. Msingi wa pili ni kuwa Kiswahili ni lugha iliyotokana na lugha kadhaa za Kibantu katika eneo la pwani.Kiisimu lugha ya Kiswahili ina utaratibumaalumu ambao ni herufi kama konsonantina irabu ambapo huweza kuunda silabi kama ba, ma, ka, la; au konsonanti, konsonanti na irabu kama kwa, gha, mwa, n.k.; au konsonanti, konsonanti, konsonati na irabu kama, mbwa, ng’we n.k.CHIMBUKO LA KISWAHILINi vigumu kusema kwa uhakika mahali ambapo ni chumbuko la Kiswahili. Pengine tunaweza kusema kuwa Kiswahili kilianzia sehemu maalumu na kuenea hadi mahali fulani. Inadaiwa kuwachimbuko la Kiswahili liko katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya lakini madai haya hayajawahi kuthibitishwa kwa hoja zenye mashiko. Ni wazi kuwa wanahistoria waliowahi kuandika kuwa mawasiliano na maelewanokati ya watu wa eneo fulani kwa kiasi fulani kulizuka lugha moja iliyoeleweka kwa watu wote katika eneo hilo. Mawasiliano ya aina hii yalizua lugha ambazo zilitofautiana kuanzia kaskazini hadi kusini mwa pwani ya Afrika Mashariki ambazo zilijulikana kama lahaja za Kiswahili. Kuanzia Kaskazinikuna lahaja ya Ci Miini ambayo huzungumzwa katika eneo la Barawa, pwani ya Somalia. Kusini zaidi kulikuwa na lahaja za Kitukuu na Kibajuni katika eneo la kusini mwa Somalia na Kaskazini mwa Kenya. Nyingine ni Kisiu sehemu za Pate, Kiamu huko Lamu, Kimvita sehemu za Mombasa, Kivumba na Kimtang’ata katika sehemu za pwani ya kaskazini mwa Tanzania, Kimakunduchi, Kihadimu, Kitumbatu sehemu za Unguja na Kipemba eneo la Pemba. Lahaja hizi zinafanana na lugha nyingineza Kibantu. Lahaja hizi zinatofautiana kidogo na Kiswahili sanifu kwa sababu Kiswahili sanifu kina maneno mengi ya mkopo. Lahaja zote hizo ni lugha zinazojitegemea.KUENEA KWA KISWAHILIKama inavyofahamika, chimbuko la Kiswahili ni upwa wote wa Afrika Mashariki. Hata hivyo lugha hii haikubaki tu katika eneo la pwani bali ilienea katika sehemu kubwa ya Afrika Mashariki. Sababu za kuenea katika sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki kulisababishwa na mambo mengi. Yako mambo yaliyosababisha kuenea kwa Kiswahili kutoka pwani hadibara. Mambo hayo ni shughuli za biashara, dini, ukoloni na hatimaye harakati za kupata uhuru. Tuangalie mchango wa mambo haya manne katika kukieneza Kiswahili.1.BiasharaKatika maelezo yaliyotolewa na wanahistoria ni kwamba wageni walikuja Pwani ya Afrika Mashariki kwa ajiliya kufanya biashara. Hata hivyo walikuwapo wenyeji wa pwani waliosafirikwenda bara kwa ajili ya kufanya biashara na wageni walipokuja waliwaonyesha njia walizowahi kuzitumiana hivyo Kiswahili kilienezwa kwa njia hiyo. Kwa maana hiyo yalikuwapo mawasiliano baina ya wenyeji wa bara napwani kwa kipindi kirefu kabla hata ya kuwasili kwa wageni. Wafanya biashara wa Kiarabu walijikita sana katika biashara ya pembe za ndovu, madini na pia utumwa. Waafrika waliokuwa wapagazi ndiyo waliokieneza Kiswahili kwa kuwasiliana na wenzao huko bara. Wafanyabiashara hawa walifika maeneoya mbali hadi Mashariki mwa Kongo naBurundi. Kutokana na umbali kutoka pwani hadi Kongo, ilitokea lahaja ya pekee iliyojulikana kama Kingwana ambayo ilitumika na kuenea katika maeneo Kongo. Kimuundo na kimsamiati lahaja ya Kigwana inafanana sana na lugha nyingine za Kibantu zina zotumika huko.Kuenezwa kwa dini za kigeniKuenea kwa dini za kigeni kama Uislamu na Ukristo kulichukua nafasi kubwa katika maisha ya wenyeji. Waarabu waliotopea katika dini ya Uislamu walitumia Kiswahili. Wahubiri wa Kiislamu walilazimika kujifunza Kiswahili kwani wenyeji hawakujua Kiarabu. Wahubiri hawa walilazimika kujifunza Kiswahili kueleza mafungu ya Korani kwa lugha inayoeleweka kwa wengi. Wahubiri hawa walianza kutumia maandishi ya Kiswahli wakitumia alfabeti za Kiarabu.Kwa kufanya hivyo, walisaidia sana kukieneza Kiswahili.Kwa upande wa dini ya Kikristo, Wamisionari hawakutaka sana kuitumialugha ya Kiswahili na waliifananisha na Uislamu. Wao walipendelea kutumia lugha za asili lakini walikosea kwani ilikuwa vigumu kujifunza lugha zote za wenyeji pamoja na kuziandika. Wangefanikiwa zaidi kama wangetumia lugha ya Kiswahili kwani ingetumiwa nawaumini wengi. Baadaye walilazimika kutumia Kiswahili kuhubiri na kuandika. Kwa kuanzia walianzisha shule za dinikwa ajili ya mafundisho ya Kikristo. Wamisionari ndiyo walioanza kutumia alfabeti za Kirumi kuandikia mahubiri yao.Kwa kuanzia wamisionari waliandika vitabu na hata kuchapisha magazeti kwa kutumia Kiswahili. Tunayo magazeti yaliyochapishwa na yalisaidia sana kukieneza Kiswahili, kwa mfano:Habari za mwezi -1988Pwani na bara - 1910Barazani - 1910Rafiki yanguHabari za Wakilindi 1903Gazeti la MsimuliziKitabu cha Wakilindi.n.k.Wakati wa UkoloniViko vipindi vitatu vya ukoloni vilivyokuwa na athari kubwa kwa lugha ya Kiswahili. Kipindi cha kwanza kilikuwa ni ukoloni wa Kiarabu. Kipindi hiki kilihusika moja kwa moja na ueneaji wa Kiswahili. Wakati huo Sultani waZanzibar alitawala Visiwa vya Pembana Unguja pamoja na ukanda wa maili kumi wa eneo la Pwani ya Kenya na Tanganyika. Kiswahli kilitumika katika kuandika na kutafsiri mafundisho ya dini ya Kiislamu.Shule za madrasa zilitumia Kiswahili kote bara na visiwani.Ukoloni wa Kijerumani ulikuta Kiswahili kimeanza kutumika kwa wingi na hivyo Wajerumani wakaanza kukitumia katika utawala wao. Shule zaawali zilizojulikana kamakindergartenzilianzishwa pamoja na vituo vya elimu watu wazima. Wafanyakazi kama Maakida, Matarishi na Maliwali walitakiwa wafahamu Kiswahili kabla yakuajiriwa. Kwa upande wa Kenya, shulenyingi za madrasa zilifundisha kwa lugha za kienyeji na baadhi kwa Kiswahili.Baada ya Wajerumani waliofuata ni Waingereza. Waingereza walifanya kazi kubwa ya kukiendeleza na kukikuza Kiswahili. Azma ya Waingereza ya kukikuza Kiswahili ni kwa ajili ya kupata wafanyakzi wa kiwango cha chinikwa ajili ya kuwapata wasaidizi katika ngazi ya chini. Kwa Waingereza, serazao hazikuruhusu Kiswahili kitumike kwakiwango cha juu kwa ajili ya kufundishia.Kiwango kilichoruhusiwa ni kufundisha shule za msingi tu. Kiswahili kilichukuliwa kama lugha ya kitwana. Lugha ya mabwana ilikuwa ni Kiingereza ambayo ilitumika kuanzia shule za sekondari na katika mawasilianokama lugha ya kazi. Hii ililandana na sera yao ya lugha katika nchi zote za Afrika Mashariki kama Kenya, Uganda na Zanzibar na Tanganyika.Mwaka 1925 ulifanyika mkutano wawakuu wa elimu wa nchi za Afrika Mashariki na kupendekeza kuwa ipatikane lugha ya Kibantu itakayotumika kama lugha ya kufundishia. Ilionekana kuwa Kiswahili ndiyo lugha itakayoweza kutumika katika kiwango cha elimu ya msingi. Tatizo lililokuwapo ni kuwa kulikuwa na lahaja nyingi za Kiswahili. Ilibidi iamuliwe kuwa lahaja ya Kiungujaitumike baada ya kusanifiwa. Uamuzi huo ulifanyika mwaka 1928 wa kukiteua Kiunguja kuwa ni lugha rasmi ya kufundishia elimu katika kiwango cha msingi. Kwa msingi huo iliundwa Kamatiya Lugha ya Afrika Mashariki (Inter-Territorial Language (Swahili) Committee ambayo ilianza kazi rasmi mwaka 1930. Kazi za kamati hii ilikuwa:1.Kusanifisha ortografia itakayotumika katika nchi za Afrika Mashariki.2.Kuweka ulinganifu wa maneno yaliyopo na yale mapya kwa kusimamiauchapishaji wa kamusi za shule.3.Kuwa na ulinganifu wa sarufi utakaotumika katika uchapishaji wa vitabu.4.Kuwatia moyo na kuwasaidia waandishi wa vitabu wanaokusudia kuandika.5.Kusahihisha vitabu vya shule ambavyo vimeshachapishwa na kufanya masahihisho pale yatakapohitajika.6.Kutafsiri kwa Kiswahili vitabu vya kiada na ziada na pale inapowezekanakuandika vitabu vipya vya kiada na ziada.7.Kuandaa vitabu vya shule vya kiada na ziada vitakavyotumika kila mwaka.Hizi ni baadhi tu ya kazi za kamati hii ya Kiswahili. Matokeo yake ni kuwapo kwa kamusi zilizotayarishwa na nyingine kuhaririwa kama:1.A Standard Kiswahili-English Dictionary2.A Standard English- Kiswahili Dictionary3.Kamusi ya Kiswahili –KiswahiliKamati hii ilipoanzishwa mwaka 1930, ilipitia vipindi mbalimbali kama vile:1.Mwaka 1930- 1947 ilikuwachini ya Magavana wa Afrika Mashariki.2.Mwaka 1948 – 1952 ilikuwa chini ya Kamati Kuu ya Afrika Mashariki3.Mwaka 1953 – 1962 ilikuwa chini ya Chuo Kikuu cha Makerere.4.1962-1964 ilikuwa chini ya Chuo Kikuu Kishiriki cha DSM katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).Taasisi nyingine iliyoanzishwa wakati wa ukoloni wa Kiingereza ilikuwa ni East African Literature Bureau. Kazi kubwa ya taasisi hii ni kuwatia moyo waandishi chipukizi kuhusu masuala ya uandishi. Kazi nyingine ni kupitia miswada ya vitabu vya Kiswahilina kuthibitisha ubora wake. Muhuri wa Ithibati ulisimamiwa na taasisi hii.Pamoja na lawama nyingi tunazotoa za kukiboronga Kiswahili, inatubidi tukiri kuwa Waingereza wamechangia sana katika ukuzaji wa Kiswahili na kutufikisha hapa tulipo sasa.Kiswahili wakati wa kupigania uhuruWakati wa kipindi cha kupigania uhuruwa nchi za Tanganyika na kwa kiasi kikubwa Kenya, Kiswahili ndiyo lugha iliyotumika kuwaunganisha wananchiwa nchi hizi. Kwa upande wa Tanganyika wakati harakati za siasazilipoanza kupamba moto hasa kipindi chaharakati za chama cha Tanganyika African Association (TAA), mbinu za chinichini zilizokuwa zikifanywazilitumia Kiswahili. Hata Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilipoanzishwa rasmi 1954, viongozi wake walikuwa wakisafiri mikoani na wilayani wakitumia Kiswahili kuwashawishi wananchi kujiunga na harakati za ukombozi. Nyimbo zilikuwa zinatungwa na kuimbwanchi nzima. Mwalimu J.K. Nyerere akiwa Mwenyekiti wa TANU alitembea nchi nzima akifuatana na wenzake na lugha mahususi iliyotumika ilikuwa ni Kiswahili. Ni sehemu chache sana ambapo lugha za kikabila zilitumikana kuhitaji mkalimani wa Kiswahili. Kwamaana hiyo, Kiswahili kilikuwa ni alama ya umoja, uzalendo na uhuru.Huko Kenya wakati wa utawala wa Uingereza, Kiswahili kilitumika kwa baadhi ya shule za msingi hasa maeneo ya pwani. Kiswahili kilitumika sana wakati wa harakati za kupigania uhuru. Wakoloni wa Uingereza walipobaini kuwa Kiswahili kinatumika kama nguzo ya umoja wa Wakenya, wakaanza kukipiga vita na kushauri lugha za makabila zitumike kama lugha za kufundishia katika shule za msingi kwa lengo la kuvunja umoja wa Wakenya.Viongozi wa KANU na hasa Hayati Mzee Jomo Kenyetta alitumia sana Kiswahili wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Kenya.Kwa upande wa Uganda, Kiswahili kilipigwa vita na Wamisionari na pia Watawala wa Baganda wakidai kuwaKiswahili kilichotumiwa sana na wafanyabiashara hasa Waarabu na kuhusishwa na dini ya Kiislamu na biashara ya watumwa. Pamoja na pingamizi zilizokuwapo, Kiswahili kiliendelea kutumika katika majeshi (ya ulinzi na polisi).Kiswahili baada ya UhuruBaada ya nchi za Afrika Masharikikupata uhuru (Tanganyika 1961, Uganda 1962, Kenya 1963 naZanzibar 1964 baada ya Mapinduzi, kila nchi ikawa na kipaumbelechake katika sera ya lugha. Nchini Tanganyika na Kenya, Kiswahili kilitumika kujenga umoja na kilifanywa kuwa ni lugha ya taifa kwa nchi hizi mbili.Kwa upande wa Tanganyika, Kiswahilikilifanywa kuwa ni lugha ya kufundishia masomo yote katika shule za msingi na pia kama somo kuanzia darasa la kwanza hadi la nane/saba. Kwa upande wa sekondari, Kiswahili kinatumika kama somo kuanzia kidato chakwanza hadi cha nne na kwa kidato cha tano na sita ilikuwa ni somo la upendeleo na si la lazima.Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanganyika katika kukiendeleza na kukikuza Kiswahili ni kwa kuanzisha asasi kadhaa kama :1.Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili(TUKI) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.2.Idara ya Kiswahili kwa ajili ya kufundisha fasihi na isimu baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuundwa kwa Sheria ya Bunge, 1970.3.Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima 19754.Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) 19765.Taasisi ya Kiswahili na Lugha zaKigeni (TAKILUKI), Zanzibar kwa ajili ya kufundisha, kukuza na kuendeleza Kiswahili na pia lugha za kigeni kama Kiarabu, Kifaransa, Kireno, Kijerumani na Kiingereza.6.Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza)Nchini Kenya:Kiswahili kilipata msukumo mkubwa baada ya Rais wa Kenya Mzee Jomo Kenyetta kutoa kauli kuwa Kiswahili kinafaa kuwa lugha rasmi kwa nchi ya Kenya na kuwa hapo baadaye kingekuwani lugha ya mawasiliano katika Bunge. Mwaka 1975 Kiswahili kilianza kutumika katika Bunge la Kenya. Ili kufanikisha azma hii, Ofisi ya Bunge la Kenya ilimtuma mtaalamu wake kuja Tanzania kuonana na viongozi wa Bakita ili kushauriana kuhusu istilahi zilizosanifiwa na kukubaliwa kuwa ni istilahi rasmi za Bakita na kulinganishaorodha hiyo na ya Kenya.Inafahamika kuwa vyuo vikuu vyote vya serikali nchini Kenya vilivyoanzishwa miaka ya 1980 vinafundisha somo laKiswahili kwa kutumia Kiswahili. Mifano hai ni Chuo Kikuu cha Nairobi, baadaye Chuo Kikuu cha Kenyatta na cha Moi. Kwa utaratibu huu idadi ya wahitimu wa Kiswahili wa kiwango cha digrii ya kwanza nchini Kenya ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wahitimu wa Kiswahili kutoka Tanzania.Kiko chama nchini Kenya kinachojulikanakama Kenya Kiswahili Association ambacho wanachama wake ni walimu pamoja na wakuza mitalaa wa Kiswahilikatika shule za sekondari. Pia wako wanafunzi wa Kiswahili walioungana nawenzao wa Tanzania na kuanzisha chama cha kukuza Kiswahili kinachojulikana kama CHAWAKAMA. Chama hiki kinawaunganisha wanafunzi wote waKiswahili wanaosoma katika vyuo vikuu vya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Huandaa semina na warsha za Kiswahili kila mwaka na hukutana kwa nchi wanachama kwa mzunguko.Suala linalotokana na mfumo wa elimu ya Kenya wa 8-4-4 unawalazimisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuchukua somo la Kiswahili kama somo la lazima. Hatuahii itawafanya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini Kenya kuona umuhimu wa lugha ya Kiswahili.Kiswahili kwa Wananchi wa Afrika MasharikiLugha ya Kiswahili ni lugha muhimu katika masuala ya siasa, elimu, uchumi, biashara na utamaduni. Kwa maana hiyo,Kiswahili kina nafasi kubwa kwa maendeleo ya Afrika Mashariki. Tumeona kuwa lugha ya Kiswahili inawaunganisha watu na kuwaletea umoja.Hakuna lugha nyingine ambayo imeenea sehemu kubwa ya Afrika Mashariki kama Kiswahili. Kwa mfumo huu ndiyo lugha inayoweza kuleta maelewano katika masuala ya kisiasa kwa wananchi wote.Katika masuala ya kiuchumi, Kiswahili kinatumika kama lugha ya mawasilano kwa upande wa biashara. Wakenya wanaweza kwenda sehemu yoyote ya vijijini nchini Tanzania na kufanya biashara bila shida. Sehemu nyingine wanazoweza kutumia Kiswahili katika biashara ni Mashariki mwa Kongo na kwa kiasi fulani Rwanda na Burundi.