Jumanne, 7 Julai 2015

MAKUNDI NENO KATIKA KISWAHILI

KIRAI

Ni kipashio cha lugha ambacho huwa na muundo wa neno moja au zaidi lakini huwa hakina muundo wa kiima na kiarifu. Muundo wa kirai huwa ni wa neno moja au zaidi ambayo huwa pamoja katika mpangilio maalumu wenye kuzingatia uhusiano wa maneno hayo na neno kuu ambalo ndio huwa linabeba aina ya kundi hilo la maneno.
            AINA ZA VIRAI
A.    Kirai nomino (KN)
Hili ni kundi la maneno ambalo hutawaliwa na nomino. Kirai nomino huundwa na maneno yafuatayo:-
o   Nomino pekee. Mfano; Asha anapika, Nyangoye anaimba, Nyegera anacheza (N)
o   Nomino mbili au zaidi zinazounganishwa. Mfano; Mhindi na Sagati wanacheza. (N+U+N)
o   Nomino na kivumishi. Mfano; Mtoto mnene amekuja, Mzee mfupi ameondoka. (N+V)
o   Kiwakilishi pekee. Mfano; Yule ameondoka, Wewe umenena, Wale waliokuja. (W)
o   Kiwakilishi na kivumishi. Mfano; Yule mvivu amerudi, Wewe mlemavu njoo. (W+V)
o   Nomino na kitenzi jina. Mfano; Mchezo wa kusisimua, Wimbo wa kupendeza. (N+Ktj)
o   Nomino na kishazi tegemezi kivumishi. Mfano; Mjukuu aliyepotea, Mheshimiwa aliyeondoka. (N+βV)
B.     Kirai kivumishi (KV)
Hiki ni kirai ambacho muundo wake umejikita katika kivumishi na maneno yanayohusiana na kivumishi katika tungo tungo hiyo. Virai hivi kwa kawaida hujibainisha zaidi kimuundo kama sehemu ya virai nomino. Virai hivi huundwa na:-
o   Kivumishi na Kirai nomino. Mfano; Mwenye mali nyingi, Wenye watoto wengi.
o   Kivumishi na kielezi. Mfano; Mzuri sana, Mweupe pee!,Mweusi tii!, Mbaya sana.
o   Kivumishi na kirai kitenzi. Mfano; Mwenye kupiga gitaa, Mwenye kupenda sana.
o   Kivumishi na kirai kiunganishi. Mfano; Nzuri ya kupendeza, Mpungufu wa akili.
C.    Kirai kitenzi (KT)
Ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi, au katika uhusiano wa kitenzi na neno au mafungu ya mengine ya maneno. Hii ina maana kwamba, neno kuu katika kirai hiki ni kitenzi. Kirai kitenzi kimeundwa na vipashio vifuatavyo:-

o   Kitenzi pekee. Mfano; amekuja, amekula, ameoga. (T)
o   Kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu. Mfano; Alikua anacheza(Ts+T), Alikua anaweza kuimba. (Ts+Ts+T)
o   Kitenzi kishirikishi na shamirisho. Mfano; Ni mtanashati, Ndiye mwizi, Sio mwelewa. (t+sh)
o   Kitenzi, jina na kielezi. Mfano; Nimepika uji asubuhi
D.    Kirai kielezi
Tofauti na aina nyingine ya virai, miundo ya virai vielezi haielekei kukitwa kwenye mahusiano ya lazima baina ya neno kuu (yaani kielezi ) na neno au fungu la maneno linaloandamana nalo. Badala yake miuundo inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika Lugha kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua zaidi neno hilo. Zaidi kirai kielezi huelezea namna, wakati, mahali na kinachofanya tendo hilo litendeke. Mfano; Mara nyingi, Sana sana, Polepole, Jana asubuhi, Kesho mchana, n.k.
E.     Kirai kihusishi
Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika mahusiano baina ya vihusishikwa, na, katika,au kwenye na fungu la maneno linaloandamana nacho. Kwa maneno menginekirai hicho ni kile ambacho neno kuu ni kihusishi. Virai vihusishi japokuwa muundo wake hufanana ila hutofautiana kimaana, zipo maana tatuambazo ni:-
a)      Pahala – kwa baba, katika kabati, kwenye lindo
b)      Utumizi – Kwa kisu, Kwa mkono
c)      Uhusika – Na Mjomba, Na Bibi.
Vilvile kirai kihusishi hutumiwa kutekeleza majukumu yafuatayo katika sentensi:-
ü  Kama kivumishi. Mfano; Penseli ya mjomba, Mkoba wa mama, Koti la babu
ü  Kama kielezi. Mfano; Tulisikiliza kwa makini, Tuliimba kwa shangwe, Tulisoma kwa juhudi
ü  Kama kiwakilishi. Mfano; La mjomba limetupwa, Ya shangazi imeuzwa, Wa nne ameondoka

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni