Jumatano, 8 Julai 2015

NGELI ZA NOMINO




    Ni namna ya kuweka majina katika makundi yanayofanana. Majina ya Kiswahili yanaweza kuwekwa katika makundi mbalimbali. Makundi hayo yamegawa na wanaisimu ya Kiswahili kwa kuzingatia maumbo ya alomofu za umoja na uwingi wa majina (kimofolojia) na kwa kuzingatia namna majina yanavyopatana na viambishi awali vya vitenzi (upatanisho wa kisarufi / kisintaksia).
1.      Kimofolojia: Katika kigezo hiki wanaisimu wameyapanga majina kulingana na alomofu za umoja na uwingi za majina hayo. Huu ni mtazamo mkongwe ambao uliofuatwa na wanasarufi wa kimapokeo wakiongozwa na Meinholf, Broomfield na Ashton mnamo miaka ya 1920 – 50. Uchambuzi ulikua kama ifuatavyo:-
1.      M-
2.      WA-
i). Majina ya viumbe vyenye uhai
ispokuwa mimea. Mfano; Mtoto – Watoto, Mzee – Wazee, Mkurya - Wakurya
ii) Majina yanayotokana na vitenzi
vinavyotaja watu. Mfano; Msomi – Wasomi, Mkulima – Wakulima, Mfanyakazi – Wafanyakazi.
3.     M-
4.      MI-
i). Majina ya mimea. Mfano; Mti – Miti, Mwembe, Miembe, Mpera – Mipera.
ii) Majina ya vitu yanayoanza na M- Mfano; Mto – Mito, Msumari – Misumari.
5.      KI-
6.      VI-
i). Majina ya vitu yanayoanza na ki- (umoja) na vi- (wingi). Mfano; Kiti – Viti, Kisu – Visu, Kikapu – Vikapu.
ii). Majina ya viumbe yanayoambishwa na ch- umoja na vy-uwingi. Mfano; Chura – Vyura, Chakula – Vyakula, Chuma – Vyuma.
7.      JI-
8.      MA-
i). Majina yanayoanza na ji- umoja na ma- uwingi. Mfano; Jicho – Macho, Jini – Majini, Jiwe – Mawe, Jina – Majina.
ii). Majina ya mkopo yenye ma- (wingi). Mfano; Bwana – Mabwana, Shati – Mashati.
iii). Majina yenye kueleza dhanna ya wingi japokuwa hayahesabiki. Maji, Majani, Maua, Maini.
9.      N-
i). Majina ambayo huanza na N inayofuatwa na konsonanti, ch-, d-,
g-, j-, z-, na y- katika umoja na wingi. Mfano; Nchi, Ndama, Ngoma, Njaa, Nzi, Nyasi.
ii). Majina yanayoanza na mb-, mv. Mfano; Mbwa, Mvi.
iii). Majina ya mkopo. Mfano; Taa, redio, Kompyuta, Kalamu.
10.  U-
11.  N-
i). Majina yote yanayoanza na U umoja na N-, mb (wingi). Mfano; Ubao – Mbao, Ulimi – Ndimi, Uso – Nyuso.
12.  U-
13.  MA-
i). Majina yote yanayoanza na uumoja na ma- wingi. Mfano; Uasi – Maasi, Uchweo – Machweo, Ugonjwa – Magonjwa.
14.  KU-
i). Majina yanayotokana na vitenzi yanayoanza na ku- (vitenzi-jina). Mfano; kucheza, Kulima, Kuimba, Kupenda.
15.  PA-

i). Huonesha mahali hasa. Mfano; Pale
16.  MU-
i). Huonesha mahali pa ndani. Mfano; Mule
17.  KU
i). Huonesha mahali pa mbali, pakubwa zaidi au popote. Mfano; Kule

UBORA WA KIGEZO CHA KIMOFOLOJIA
                   I.            Uwezekano wa kuzigawa nomino nyingi za Kiswahili ni mkubwa kwa kuwa nyingi zimegawanyika katika maumbo hayo ya umojha na uwingi.
                II.            Ni kigezo muhimu kwani kinajikita zaidi katika nomino na kivumishi chake peke yake hakigusi aina nyingine ya neno tofauti na kigeso cha kisintaksia ambacho hugusa hadi kitenzi.
             III.            Huwasaidia wanasarufi linganishi kuonesha uhusiano wa lugha za vikoa kimoja.

        UPUNGUFU WA KIGEZO HIKI.
                               I.            Kuna viambishi katika ngeli tofauti vinavyofanana. Mfano Kiambishi M- kinajitokeza katika ngeli ya 1 na 3 na MA- inajitokeza katika ngeli ya 8 na 13.
                            II.            Kuna nomino nyingine ambazo hazijidhihirishi katika umoja na uwingi. Mfano ngeli ya 8 na 9.
2.      Kigezo cha sintaksia /upatanisho wa kisarufi:
   Huu ni mtazamo wa kisasa wa uainishaji wa ngeli ambao umeyagawa majina katika makundi kulingana na upatanisho wa kisarufi kat ya jina na viambishi awali vilivyo katika vitenzi. Kwa mujibu wa mtazamo huu, majina yamepangwa katika makundi tisa ambayo ni:-
1.      A -WA
Mfano; Mtoto anacheza / Watoto wanacheza.
            Mzee analima / Wazee wanalima.
             Mwanafunzi anasoma / Wanafunzi wanasoma.
2.      U – I
Mfano; Mkufu umekatika / Mikufu imekatika.
             Mji umevamiwa / Miji imevamiwa.
             Mkaa umemwagika / Mikaa imemwagika.
3.      LI – YA
Mfano; Gogo limevunjika / Magogo yamevunjika.
             Gari limepotea / Magari yamepotea.
              Jiko limewaka / Majiko yamewaka
4.      KI – VI
Mfano;   Kiapo kimekiukwa / Viapo vimekiukwa.
               Kilima kimesawazishwa / Vilima vimesawazishwa.
               Kikongwe kimeuawa / Vikongwe vimeuawa.
5.      I – ZI
Mfano; Ng’ombe imechinjwa / Ng’ombe zimechinjwa.
             Nguo imechanika / Nguo zimechanika.
              Nchi imekosa amani / Nchi zimekosa amani.
6.      U – ZI
Mfano; Ubao umeandikika / Mbao zimeandikika.
             Ukuta umeanguka / Kuta zimeanguka.
             Uzi umetumika / Nyuzi zimetumika.
7.      U – YA
Mfano; Ugonjwa unatisha / Magonjwa yanatisha.
             Uasi umekithiri / Maasi yamekithiri.
8.      KU
Mfano; Kulima kunachosha.
             Kuimba kwake kunafurahisha.
           Kufurahi kwake kumemponya.
9.      PA – MU - KU
Mfano; Hapa pananuka.
             Humu mna nzi.
             Kule kumebomoka.
UBORA WA KIGEZO CHA KISINTAKSIA
n  Unajitosheleza kwa kuwa kila jina inakuwa na upatanishi wake katika kitenzi.
UPUNGUFU WA KIGEZO HIKI
I.                   Kuna viambishi vinavyojirudia. Mfano, U- kimejitokeza katika ngeli ya 2, 6 na 7.
II.                Huyaweka majina yenye maumbo tofauti katika ngeli moja.
III.             Kunaweza kuwa na utata katika upatanisho kwa baadhi ya majina kama “makala”
      Mfano; Makala yamechapishwa.
                  Makala imechapishwa.
Sentensi hizo zote zinatumika ila hatuna wingi wa makala katika Kiswahili

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni