Jumatano, 8 Julai 2015

KISHAZI KATIKA KISWAHILI



1.      KISHAZI
Ni aina ya tungo ambayo huwa na kitenzi ndani yake, kitenzi hicho kinaweza kikawa kinakamilisha maana au kisiwe kinajikamilisha kimaana. Kitenzi ambacho huwa kinakamilisha maana huwa ni kitenzi kikuu (T), na kile kisichokuwa kinatoa taarifa kamili huwa ni kitenzi kisaidizi (TS). Kwa mujibu huo tunapata aina mbili za kishazi yaani kishazi huru na kishazi tegemezi.
A.    Kishazi huru (K/Hr)
Aina hii ya kishazi huwa na tabia ya kutoa taarifa ambayo huwa ni kamili katika tungo, hubeba kitenzi kikuu au kishirikishi ndani yake. Kishazi hiki huwa hakihitaji maelezo ya ziada ili kukamilisha maana au taarifa kusudiwa na pia huweza kujitegemea kama sentensi kamili na huwa na muundo wa kiima na kiarifu.
Mfano; Mtoto / anacheza mpira
                  K                     A
            Mwanafunzi / anasoma kitabu
                  K                     A
            Mwanaume / anakufahamu
                  K                     A
           Mwanafunzi /. ni mpole
                  K                     A
B. Kishazi tegemezi (K/ Tg)
Aina hii ya kishazi huwa haitoi taarifa iliyokamili badala yake hutegemea kishazi huru ili kukamilisha taarifa iliyokusudiwa na msemaji. Kishazi hiki hutawaliwa na kitenzi kisaidizi. Kishazi tegemezi kwa upekee wake hakiwezi kutoa taarifa iliyokusudiwa. Vishazi tegemezi hushuka hadhi na kuwa na hadhi ya kikundi cha maneno (kirai).
Mfano;      Mtoto unayemjua
                  Mwanafunzi anayesoma
                  Mahali alipoingia
                  Mama alipomchapa
                  Kaka aliporudi
Vishazi hivyo hapo juu havitoi taarifa iliyokamili ila tunapoviweka pamoja na vishazi huru taarifa iliyokusudiwa hukamilika. Tazama hapa chini:-
Mfano;       Mtoto unayemjua ameondoka
                  Mwanafunzi anayesoma atafaulu
                  Mahali alipoingia ni pachafu
                  Mama alipomchapa aliondoka
                  Kaka aliporudi alinifurahisha
Sifa za kishazi tegemezi
                    i.            Hakikamilishi taarifa pasipokuwepo na kishazi huru
Mfano;       Mtoto anayecheza mpira ameumia
                  Mvulana aliyefaulu mtihani amefurahi
                  Mama alipomkaribisha aliingia ndani
                  ii.            Kinaweza kuondolewa katika tungo bila kuathiri taarifa kusudiwa.
Mfano;      mtoto aliyeugua amepona
                  Mtoto amepona
                  Mama uliyemsalimia pale ameondoka jana.
                  Mama ameondoka jana
                iii.            Hutambulishwa na vitambulishi vya urejeshi vinavyopachikwa katika vitenzi.
Mfano; Anayesoma, Alichookota, Uliokatika, Iliyoibiwa, Alipoingia n.k.
                iv.            Vilevile kashazi tegemezi hutambulishwa na viunganishi tegemezi kwamba, ili, ili kwamba, kwa sababu, mzizi wa amba na kiambishi cha masharti.
Mfano;       Mama alisema kwamba motto ameumia
                  Mvulana ambaye ni kaka yangu amerejea nyumbani
                  Akijua atanichapa
            Vishazi tegemezi vipo vya aina mbili kutokana na majukumu yake kimuundo
A.    Kishazi tegemezi kivumishi (bV)
Kishazi tegemezi kivumishi hufanya kazi ya kuvumisha nomino katika tungo.
      Mfano;            Baba anayenijali
                              Mbwa aliyepotea
                              Mwanafunzi aliyefariki
                              Uliyemuona pale
                              Aliyempenda sana

B.     Kishazi tegemezi kielezi (bE)
 Kishazi hiki hufanya kazi ya kueleza tendo katika tungo na hujitokeza kueleza dhima tofauti tofauti kama ifuatavyo:-
ü  Kueleza mahali tendo linapofanyika. Mfano; Alipoingia (mahali dhahiri), Alimochungulia (ndani ya kitu Fulani), Alikoelekea (mahali pasipo dhahiri)
ü  Kueleza wakati wa tendo. Mfano; Tulipotoka, Alipomchapa, Walipomsema n.k.
ü  Kueleza masharti katika tendo. Mfano; Akirudi, Angekuja, Angelimpiga, Angalijua n.k.
ü  Kueleza namna tendo linavyofanyika. Mfano; Alivyoimba, Walivyopendeza, Tulivyomsifu.
ü  Kueleza kasoro katika kukamilisha tendo. Mfano; Ingawa amesoma, Licha ya kufaulu, Japokua amependekezwa.
ü  Kueleza sababu ya kufanyika kwa tendo. Mfano; Kwa sababu alipendeza, Kwa kuwa hujafaulu, Kwa vile umenisomesha.

Maoni 1 :

  1. Je namna ya kutenganisha vishazi huru na tegemezi?????????

    JibuFuta